20. Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,
21. Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.
22. Je! Hamniogopi mimi? Asema BWANA; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.
23. Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.
24. Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche BWANA, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.
25. Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.
26. Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu.
27. Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali.
28. Wamewanda sana, wang’aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji.
29. Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?