Yer. 5:19-30 Swahili Union Version (SUV)

19. Tena itakuwa mtakapouliza, BWANA ametutenda mambo hayo yote kwa sababu gani? Ndipo utakapowaambia, Vile vile kama ninyi mlivyoniacha mimi, na kuwatumikia miungu mingine katika nchi yenu wenyewe, ndivyo mtakavyowatumikia wageni katika nchi isiyo yenu.

20. Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,

21. Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.

22. Je! Hamniogopi mimi? Asema BWANA; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.

23. Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.

24. Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche BWANA, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.

25. Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.

26. Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu.

27. Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali.

28. Wamewanda sana, wang’aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji.

29. Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?

30. Jambo la ajabu, la kuchukiza, limetokea katika nchi hii!

Yer. 5