15. Angalia, nitaleta taifa juu yenu litokalo mbali sana, Ee nyumba ya Israeli, asema BWANA; ni taifa hodari, ni taifa la zamani sana, taifa ambalo hujui lugha yake, wala huyafahamu wasemayo.
16. Podo lao ni kaburi wazi, ni mashujaa wote pia.
17. Nao watakula mavuno yako, na mkate wako, ambao iliwapasa wana wako na binti zako kuula; watakula makundi yako ya kondoo na ya ng’ombe; watakula mizabibu yako na mitini yako; wataiharibu miji yako yenye boma, uliyokuwa ukiitumainia, naam, wataiharibu kwa upanga.
18. Lakini hata katika siku zile, asema BWANA, sitawakomesha ninyi kabisa.
19. Tena itakuwa mtakapouliza, BWANA ametutenda mambo hayo yote kwa sababu gani? Ndipo utakapowaambia, Vile vile kama ninyi mlivyoniacha mimi, na kuwatumikia miungu mingine katika nchi yenu wenyewe, ndivyo mtakavyowatumikia wageni katika nchi isiyo yenu.
20. Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,
21. Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.
22. Je! Hamniogopi mimi? Asema BWANA; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.
23. Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.
24. Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche BWANA, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.
25. Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.
26. Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu.
27. Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali.
28. Wamewanda sana, wang’aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji.