1. Pigeni mbio huku na huku katika njia za Yerusalemu, mkaone sasa, na kujua, na kutafuta katika viwanja vyake, kwamba mwaweza kumpata mtu mmoja, kwamba yuko mtu mmoja awaye yote atendaye kwa haki, atafutaye uaminifu; nami nitausamehe mji huo.
2. Na wajaposema, Kama BWANA aishivyo, hakika waapa kwa uongo.
3. Ee BWANA, macho yako je! Hayaangalii uaminifu? Umewapiga, lakini hawakuhuzunika; umewakomesha, lakini wamekataa kurudiwa wamefanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba wamekataa kurudi.
4. Ndipo nikasema, Hakika, hawa ni maskini; ni wajinga hawa; maana hawaijui njia ya BWANA, wala hukumu ya Mungu wao;
5. nitawaendea watu wakubwa, nami nitasema nao; kwa maana hao wanaijua njia ya BWANA, na hukumu ya Mungu wao. Bali hawa kwa nia moja wameivunja nira, na kuvikata vifungo.
6. Basi, kwa hiyo, simba atokaye mwituni atawaua, mbwa-mwitu wa jioni atawateka, chui ataivizia miji yao, kila mtu atokaye humo atararuliwa vipande vipande; kwa sababu makosa yao ni mengi, na kurudi nyuma kwao kumezidi.
7. Nawezaje kukusamehe? Watoto wako wameniacha mimi, na kuapa kwa hao ambao si miungu; nilipokuwa nimewashibisha chakula, walizini, wakakutana wengi pamoja katika nyumba za makahaba.
8. Walikuwa kama farasi walioshiba wakati wa asubuhi; kila mmoja akalia kwa kutamani mke wa mwenzake.