Yer. 48:1-14 Swahili Union Version (SUV)

1. Habari za Moabu. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ole wake Nebo! Kwa maana umeharibika; Kiriathaimu umeaibishwa, umetwaliwa; Misgabu umeaibishwa, nao umebomolewa.

2. Sifa za Moabu haziko tena; katika Heshboni wameazimia mabaya juu yake, Haya! Njoni, na tumkatilie mbali asiwe taifa. Wewe nawe, Ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.

3. Sauti ya kilio toka Horonaimu,Ya kutekwa na uharibifu mkuu.

4. Moabu umeharibika;Wadogo wake wamewasikiza watu kilio.

5. Kwa maana watu wapandapo huko LuhithiWatapanda wasiache kulia;Nao watu watelemkapo huko HoronaimuWameisikia huzuni ya kilio cha uharibifu.

6. Haya! Kimbieni! Jiokoeni nafsi zenu!Mkawe kama mtu aliye mkiwa.

7. Maana, kwa kuwa umeyatumainia matendo yako, na hazina zako, wewe nawe utatwaliwa; na Kemoshi atatoka aende katika uhamisho, makuhani wake na wakuu wake pamoja.

8. Naye mwenye kuteka nyara atakuja juu ya kila mji, wala hapana mji utakaookoka; bonde nalo litaangamia, nayo nchi tambarare itaharibiwa; kama BWANA alivyosema.

9. Mpe Moabu mabawa, apate kuruka na kwenda zake; na miji yake itakuwa ukiwa, isiwe na mtu wa kukaa ndani yake.

10. Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu.

11. Moabu amestarehe tangu ujana wake, naye ametulia juu ya sira zake, wala hakumiminwa kutoka chombo kimoja kutiwa chombo kingine, wala hakwenda kufungwa; kwa hiyo ladha yake anakaa nayo, wala harufu yake haikubadilika.

12. Basi, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo nitampelekea wamiminao, nao watammimina, nao watamwaga vyote vilivyomo vyomboni mwake, na kuzivunja chupa zake vipande vipande.

13. Na Moabu ataona haya kwa ajili ya Kemoshi, kama nyumba ya Israeli ilivyoona haya kwa ajili ya Betheli, matumaini yao.

14. Mwasemaje ninyi, Sisi tu mashujaa, watu hodari wa vita.

Yer. 48