9. Je! Mmeusahau uovu wa baba zenu, na uovu wa wafalme wa Yuda, na uovu wa wake zao, na uovu wenu wenyewe, na uovu wa wake zenu, walioutenda katika nchi ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
10. Hawajanyenyekea hata leo, wala hawakuogopa, wala hawakuenenda katika sheria yangu, wala katika amri zangu, nilizoweka mbele yenu, na mbele ya baba zenu.
11. Basi, kwa sababu hiyo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaelekeza uso wangu juu yenu, ili niwaletee mabaya, hata kukatilia mbali Yuda yote.
12. Nami nitawatwaa mabaki ya Yuda, walioelekeza nyuso zao kuiingia nchi ya Misri, wakae huko, nao wataangamia wote pia; wataanguka katika nchi ya Misri; wataangamia kwa upanga, na kwa njaa; watakufa, tangu wadogo hata wakubwa, kwa upanga, na kwa njaa; nao watakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu.
13. Kwa maana nitawaadhibu wakaao katika nchi ya Misri, kama nilivyouadhibu Yerusalemu, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni;