3. kwa sababu ya uovu wao, waliotenda ili kunikasirisha, kwa kuwa walikwenda kufukiza uvumba, na kuwatumikia miungu mingine, ambao hawakuwajua, wao, wala ninyi, wala baba zenu.
4. Tena nalituma kwenu watumishi wangu wote, manabii, nikiamka mapema na kuwatuma, nikisema, Basi ninyi; msilifanye chukizo hili linichukizalo.
5. Lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, ili wageuke na kuacha uovu wao, wasifukizie uvumba miungu mingine.
6. Kwa sababu hiyo ghadhabu yangu, na hasira yangu, zilimwagika, nazo ziliwaka katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, na miji hiyo imeachwa ukiwa, na kuharibika, kama ilivyo leo.
7. Basi, sasa, BWANA, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa nini mnafanya uovu huu mkubwa juu ya nafsi zenu wenyewe, kujikatilia mbali mwanamume na mwanamke, mtoto mchanga na anyonyaye, mtoke kati ya Yuda, msijiachie mtu abakiye;
8. kwa kuwa mnanikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, mkifukizia uvumba miungu mingine katika nchi ya Misri, mlikokwenda kukaa ugenini; mpate kukatiliwa mbali, na kuwa laana, na aibu, katika mataifa yote ya dunia?