Yer. 44:13-23 Swahili Union Version (SUV)

13. Kwa maana nitawaadhibu wakaao katika nchi ya Misri, kama nilivyouadhibu Yerusalemu, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni;

14. hata katika watu wale wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili wakae huko, hapatakuwa na mtu ye yote atakayepona, wala atakayesalia, na kupata kurudi nchi ya Yuda, ambayo wanatamani kurudi ili kukaa huko; maana hapana atakayerudi, ila wao watakaopona.

15. Ndipo watu wote waliojua ya kuwa wake zao waliwafukizia uvumba miungu mingine, na wanawake wote waliosimama karibu, mkutano mkubwa, yaani, watu wote waliokaa katika nchi ya Misri, katika Pathrosi, wakamjibu Yeremia, wakisema,

16. Neno lile ulilotuambia kwa jina la BWANA, sisi hatutakusikiliza.

17. Lakini bila shaka tutalitimiza kila neno lililotoka katika vinywa vyetu, kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, kama tulivyotenda sisi, na baba zetu, na wafalme wetu, na wakuu wetu, katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu; maana wakati huo tulikuwa na chakula tele, na kufanikiwa, wala hatukuona mabaya.

18. Lakini tulipoacha kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, tumepungukiwa na vitu vyote; na kuangamizwa kwa upanga, na kwa njaa.

19. Nasi tulipomfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, je! Tulimfanyizia mikate, ili kumwabudu, na kummiminia mamiminiko, waume zetu wasipokuwapo?

20. Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake, yaani, watu wote waliompa jibu lile, akisema,

21. Uvumba mliofukiza katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ninyi, na baba zenu, wafalme wenu, na wakuu wenu, na watu wa nchi, je! BWANA hakuwakumbuka watu hao? Je! Jambo hili halikuingia moyoni mwake?

22. Hata BWANA asiweze kuvumilia tena, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu, na kwa sababu ya machukizo mliyoyafanya; kwa sababu hiyo nchi yenu imekuwa ukiwa, na ajabu, na laana, isikaliwe na mtu kama ilivyo leo.

23. Kwa sababu mmefukiza uvumba, na kwa sababu mmetenda dhambi juu ya BWANA, wala hamkuitii sauti ya BWANA, wala hamkwenda katika torati yake, wala katika amri zake, wala katika shuhuda yake; ndiyo maana mabaya haya yamewapata kama ilivyo leo.

Yer. 44