Yer. 43:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Ikawa Yeremia alipokwisha kuwaambia watu wote maneno yote ya BWANA, Mungu wao, ambayo BWANA, Mungu wao, amemtuma kwao, yaani, maneno hayo yote,

2. ndipo Azaria, mwana wa Hoshaya, na Yohana mwana wa Karea, na watu wote wenye kiburi wakanena, wakimwambia Yeremia, Unasema uongo; BWANA, Mungu wetu, hakukutuma useme, Msiende Misri kukaa huko;

3. bali Baruku, mwana wa Neria, akushawishi kinyume chetu, ili kututia katika mikono ya Wakaldayo, ili watuue, na kutuchukua mateka mpaka Babeli.

4. Basi Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi, na watu wote hawakuitii sauti ya BWANA, kwamba wakae katika nchi ya Yuda.

5. Lakini Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi, wakawatwaa wote waliosalia wa Yuda, waliokuwa wamerudi kutoka taifa zote walikofukuzwa, wakae katika Yuda;

6. wanaume, na wanawake, na watoto, na binti za mfalme, na kila mtu ambaye Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, amemwacha pamoja na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, pia na Yeremia, nabii, na Baruku, mwana wa Neria;

7. wakaingia nchi ya Misri; maana hawakuitii sauti ya BWANA; wakafika hata Tahpanesi.

8. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia huko Tahpenesi, kusema,

9. Twaa mawe makubwa mikononi mwako, ukayafiche ndani ya chokaa ya kazi ya matofali, penye maingilio ya nyumba ya Farao huko Tahpanesi, machoni pa watu wa Yuda;

Yer. 43