17. Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao.
18. Maana BWANA wa majeshi Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama hasira yangu, na ghadhabu yangu, ilivyomwagwa juu ya hao wakaao Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu, mtakapoingia Misri; nanyi mtakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu; wala hamtapaona mahali hapa tena.
19. BWANA asema katika habari zenu, enyi mabaki ya Yuda, Msiingie Misri; jueni sana ya kuwa nimewashuhudia hivi leo.
20. Maana mmetenda kwa hila juu ya nafsi zenu wenyewe; kwa kuwa mmenituma kwa BWANA, Mungu wenu, mkisema, Utuombee kwa BWANA, Mungu wetu, ukatufunulie sawasawa na yote atakayoyanena BWANA, Mungu wetu, nasi tutayatenda;
21. nami nimewafunulia haya leo; lakini ninyi hamkuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu, katika neno lo lote ambalo amenituma kwenu.
22. Basi, sasa jueni sana ya kuwa mtakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, katika mahali pale mnapopatamani kwenda na kukaa.