7. Kisha, wakuu wote wa majeshi waliokuwa katika bara, wao na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, kuwa liwali juu ya nchi, na kwamba amemkabidhi wanaume na wanawake na watoto, na baadhi ya maskini wa nchi wasiochukuliwa mateka Babeli;
8. ndipo wakamwendea Gedalia huko Mizpa; nao ni hawa, Ishmaeli, mwana wa Nethania, na Yohana na Yonathani, wana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanhumethi, na wana wa Efai, Mnetofa, na Yezania, mwana wa Mmaaka, wao na watu wao.
9. Na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, akawaapia wao na watu wao, akisema, Msiogope kuwatumikia Wakaldayo; kaeni katika nchi, mkamtumikie mfalme wa Babeli; nayo itawafaa.
10. Na mimi, tazama, nitakaa Mizpa, ili nisimame mbele ya Wakaldayo watakaotujilia; lakini ninyi chumeni divai, na matunda ya wakati wa jua, na mafuta, mkaviweke vitu hivyo katika vyombo vyenu, mkakae katika miji yenu mliyoitwaa.
11. Kadhalika waliposikia Wayahudi wote, waliokuwa katika Moabu, na kati ya wana wa Amoni, na hao waliokuwa katika Edomu, na hao waliokuwa katika nchi zote, ya kuwa mfalme wa Babeli amewaachia Yuda mabaki, na ya kuwa amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, juu yao;
12. basi, Wayahudi wote wakarudi kutoka kila mahali walikofukuzwa wakaenda mpaka nchi ya Yuda, wakamwendea Gedalia huko Mizpa, wakakusanya divai, na matunda ya wakati wa jua mengi sana.
13. Tena Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi ya barani, wakamwendea Gedalia huko Mizpa,
14. wakamwambia, Je! Una habari wewe ya kuwa Baalisi, mfalme wa wana wa Amoni, amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania, akuue? Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, hakusadiki neno hili.
15. Basi, Yohana, mwana wa Karea, akamwambia Gedalia huko Mizpa kwa siri, akisema, Niache niende nikampige Ishmaeli, mwana wa Nethania, wala hapana mtu atakayejua jambo hili; kwani akuue wewe, hata wakatawanyike Wayahudi waliokukusanyikia, na mabaki ya Yuda wakaangamie?
16. Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, akamwambia Yohana, mwana wa Karea, Usilitende jambo hili, maana unamsingizia Ishmaeli.