17. Kama watu walindao shamba, wameuzunguka wauhusuru; kwa sababu ameniasi mimi, asema BWANA.
18. Njia yako na matendo yako yamekupatia haya; huu ndio uovu wako; kwa maana ni uchungu, hakika unafikilia hata moyo wako.
19. Mtima wangu, mtima wangu! Naumwa katika moyo wangu wa ndani; moyo wangu umefadhaika ndani yangu; siwezi kunyamaza; kwa sababu umesikia, Ee nafsi yangu, sauti ya tarumbeta, mshindo wa vita.
20. Uangamivu baada ya uangamivu umetangazwa; kwa maana nchi yote imeharibika; hema zangu zimetekwa nyara ghafula, na mapazia yangu katika dakika moja.
21. Niione bendera hata lini, na kuisikia sauti ya tarumbeta?
22. Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.
23. Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru.
24. Naliiangalia milima, na tazama, ilitetemeka, na milima yote ilisogea huko na huko.
25. Nikaangalia, na tazama, hapakuwa na mtu hata mmoja, na ndege wote wa angani wamekwenda zao.
26. Nikaangalia, na tazama, shamba lililozaa sana limekuwa ukiwa, na miji yake yote ilikuwa imebomoka mbele za BWANA, na mbele za hasira yake kali.
27. Maana BWANA asema hivi, Nchi yote itakuwa ukiwa; lakini sitaikomesha kabisa.
28. Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na mbingu zitakuwa nyeusi; kwa sababu mimi nimeyanena haya, na kuyakusudia, wala sikujuta wala mimi sitarudi nyuma niyaache.
29. Mji mzima unakimbia, kwa sababu ya mshindo wa wapanda farasi na wenye pinde wanaingia vichakani, wanapanda juu ya majabali; kila mji umeachwa, hapana hata mtu mmoja akaaye ndani yake.
30. Na wewe, utakapotekwa, utafanyaje? Ujapojivika mavazi mekundu, ujapojipamba mapambo ya dhahabu, ujapojitia wanja machoni, unajifanya kuwa mzuri bure tu; wapenzi wako wanakudharau; wanakutafuta roho yako.
31. Kwa maana nimesikia sauti, kama sauti ya mwanamke wakati wa utungu wake, na sauti yake aumwaye, kama mwanamke azaaye mtoto wake wa kwanza, sauti ya binti Sayuni, atwetaye kupata pumzi, na kunyosha mikono yake, akisema, Ole wangu, sasa! Kwa maana roho yangu inazimia mbele ya wauaji.