17. Kama watu walindao shamba, wameuzunguka wauhusuru; kwa sababu ameniasi mimi, asema BWANA.
18. Njia yako na matendo yako yamekupatia haya; huu ndio uovu wako; kwa maana ni uchungu, hakika unafikilia hata moyo wako.
19. Mtima wangu, mtima wangu! Naumwa katika moyo wangu wa ndani; moyo wangu umefadhaika ndani yangu; siwezi kunyamaza; kwa sababu umesikia, Ee nafsi yangu, sauti ya tarumbeta, mshindo wa vita.
20. Uangamivu baada ya uangamivu umetangazwa; kwa maana nchi yote imeharibika; hema zangu zimetekwa nyara ghafula, na mapazia yangu katika dakika moja.
21. Niione bendera hata lini, na kuisikia sauti ya tarumbeta?
22. Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.
23. Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru.
24. Naliiangalia milima, na tazama, ilitetemeka, na milima yote ilisogea huko na huko.