Yer. 4:11-23 Swahili Union Version (SUV)

11. Wakati ule watu hawa na Yerusalemu wataambiwa neno hili, Upepo wa moto utokao katika vilele vya nyikani visivyo na miti, ukimwelekea binti ya watu wangu, hauwi upepo wa kupepeta, wala upepo wa kutakasa;

12. ni upepo wa nguvu kuliko hizo utakaokuja kwa ajili yangu; sasa mimi nitatoa hukumu juu yao.

13. Tazama atapanda juu kama mawingu, na magari yake ya vita yatakuwa kama kisulisuli; farasi zake ni wepesi kuliko tai. Ole wetu, kwa sababu tumeharibika.

14. Ee Yerusalemu, jioshe moyo wako usiwe na uovu, upate kuokoka. Mawazo yako mabaya yatakaa ndani yako hata lini?

15. Maana sauti yatangaza habari toka Dani, yahubiri uovu toka vilima vya Efraimu;

16. Wapasheni mataifa habari; angalieni, hubirini juu ya Yerusalemu, ya kwamba walinzi wanatoka katika nchi ya mbali, wanatoa sauti yao juu ya miji ya Yuda.

17. Kama watu walindao shamba, wameuzunguka wauhusuru; kwa sababu ameniasi mimi, asema BWANA.

18. Njia yako na matendo yako yamekupatia haya; huu ndio uovu wako; kwa maana ni uchungu, hakika unafikilia hata moyo wako.

19. Mtima wangu, mtima wangu! Naumwa katika moyo wangu wa ndani; moyo wangu umefadhaika ndani yangu; siwezi kunyamaza; kwa sababu umesikia, Ee nafsi yangu, sauti ya tarumbeta, mshindo wa vita.

20. Uangamivu baada ya uangamivu umetangazwa; kwa maana nchi yote imeharibika; hema zangu zimetekwa nyara ghafula, na mapazia yangu katika dakika moja.

21. Niione bendera hata lini, na kuisikia sauti ya tarumbeta?

22. Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.

23. Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru.

Yer. 4