12. Mtwae, umtunze sana, wala usimtende neno baya lo lote; lakini umtendee kama atakavyokuambia.
13. Basi Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, na Nebu-Shazbani, mkuu wa matowashi, na Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu, na maakida wakuu wote wa mfalme wa Babeli,
14. wakatuma watu wakamwondoa Yeremia katika uwanda wa walinzi, wakamweka katika mikono ya Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ili ampeleke nyumbani kwake; basi akakaa pamoja na hao watu.
15. Basi neno la BWANA likamjia Yeremia, wakati ule alipokuwa amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
16. Haya! Enenda ukaseme na Ebedmeleki, Mkushi, kusema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaupatiliza mji huu maneno yangu kwa mabaya, wala si kwa mema; nayo yatatimizwa mbele yako katika siku hiyo.
17. Lakini nitakuokoa wewe katika siku hiyo, asema BWANA; wala hutatiwa katika mikono ya watu wale unaowaogopa.
18. Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema BWANA.