9. Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji.
10. Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.
11. Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamtelemshia Yeremia shimoni kwa kamba.
12. Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo.
13. Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.
14. Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya BWANA; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lo lote.