12. ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu.
13. Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, akida wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo.
14. Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimsadiki; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu.
15. Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza.
16. Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi;
17. ndipo Sedekia, mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa BWANA? Yeremia akasema, Liko. Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli.
18. Pamoja na haya Yeremia akamwambia mfalme Sedekia, Nimefanya kosa gani juu yako, au juu ya watumishi wako, au juu ya watu hawa, hata mkanitia gerezani?