1. Na Sedekia, mwana wa Yosia, akamiliki badala ya Konia, mwana wa Yehoyakimu, ambaye Nebukadreza amemmilikisha katika nchi ya Yuda.
2. Lakini yeye, wala watumishi wake, wala watu wa nchi, hawakuyasikiliza maneno ya BWANA aliyonena kwa kinywa cha nabii Yeremia.
3. Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa BWANA, Mungu wetu.
4. Basi Yeremia alikuwa akiingia na kutoka kati ya watu; kwa maana walikuwa hawakumfunga gerezani.
5. Na jeshi la Farao lilikuwa limetoka nchi ya Misri; na Wakaldayo waliohusuru Yerusalemu, waliposikia habari zao, wakavunja kambi yao mbele ya Yerusalemu.
6. Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia, kusema,
7. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe.
8. Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza.
9. BWANA asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha.
10. Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu.
11. Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao,
12. ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu.