Yer. 36:22-31 Swahili Union Version (SUV)

22. Basi mfalme alikuwa ameketi katika nyumba iliyotumika wakati wa baridi, mwezi wa kenda; na pale palikuwa na moto wa makaa mbele yake.

23. Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.

24. Lakini hawakuogopa, wala hawakurarua mavazi yao, wala mfalme, wala watumishi wake hata mmoja waliosikia maneno hayo yote.

25. Hata hivyo Elnathani, na Delaya, na Gemaria, walikuwa wamemsihi mfalme asiliteketeze gombo lile, lakini hakukubali kuwasikia.

26. Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini BWANA aliwaficha.

27. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, hapo mfalme alipokuwa amekwisha kuliteketeza gombo lile, na maneno yale aliyoyaandika Baruku, yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, kusema,

28. Haya! Twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza.

29. Na katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema, BWANA asema hivi, Umeliteketeza gombo hili, ukisema, Mbona umeandika ndani yake, ukisema, Bila shaka mfalme wa Babeli atakuja, na kuiharibu nchi hii, na kukomesha mwanadamu na mnyama pia ndani yake?

30. Basi, BWANA aseme hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi.

31. Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza.

Yer. 36