18. Baruku akawajibu, Alinitamkia maneno haya yote kwa kinywa chake, nami nikayaandika kwa wino kitabuni.
19. Ndipo hao wakuu wakamwambia Baruku, Enenda ukajifiche, wewe na Yeremia, wala mtu asipajue mlipo.
20. Wakaenda kwa mfalme uwandani; lakini walikuwa wameliweka lile gombo katika chumba cha Elishama, mwandishi wakayanena maneno hayo yote masikioni mwa mfalme.
21. Basi, mfalme akamtuma Yehudi aende akalilete lile gombo; naye akalitoa katika chumba cha Elishama, mwandishi. Yehudi akalisoma masikioni mwa mfalme, na masikioni mwa wakuu waliosimama mbele ya mfalme.
22. Basi mfalme alikuwa ameketi katika nyumba iliyotumika wakati wa baridi, mwezi wa kenda; na pale palikuwa na moto wa makaa mbele yake.
23. Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.
24. Lakini hawakuogopa, wala hawakurarua mavazi yao, wala mfalme, wala watumishi wake hata mmoja waliosikia maneno hayo yote.
25. Hata hivyo Elnathani, na Delaya, na Gemaria, walikuwa wamemsihi mfalme asiliteketeze gombo lile, lakini hakukubali kuwasikia.
26. Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini BWANA aliwaficha.
27. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, hapo mfalme alipokuwa amekwisha kuliteketeza gombo lile, na maneno yale aliyoyaandika Baruku, yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, kusema,
28. Haya! Twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza.