12. akashuka, akaingia katika nyumba ya mfalme, katika chumba cha mwandishi, na, tazama, wakuu wote wameketi humo, nao ni hawa, Elishama, mwandishi, na Delaya, mwana wa Shemaya, na Elnathani, mwana wa Akbori, na Gemaria, mwana wa Shafani, na Sedekia, mwana wa Hanania, na wakuu wote.
13. Naye Mikaya akawaeleza maneno yote aliyoyasikia, hapo Baruku alipokuwa akikisoma kitabu masikioni mwa watu.
14. Basi, wakuu wote wakamtuma Yehudi, mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, aende kwa Baruku, kumwambia, Litwae mkononi mwako gombo lile ulilolisoma masikioni mwa watu, uje huku. Basi, Baruku, mwana wa Neria, akalitwaa gombo lile mkononi mwake, akaenda kwao.
15. Nao wakamwambia, Keti sasa, ukalisome masikioni mwetu. Basi, Baruku akalisoma masikioni mwao.
16. Ikawa, walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana kwa hofu, wakamwambia Baruku, Hatuna budi kumwambia mfalme maneno haya yote.
17. Wakamwuliza Baruku, wakisema, Tuambie sasa; ulipataje kuyaandika maneno haya yote kinywani mwake?
18. Baruku akawajibu, Alinitamkia maneno haya yote kwa kinywa chake, nami nikayaandika kwa wino kitabuni.
19. Ndipo hao wakuu wakamwambia Baruku, Enenda ukajifiche, wewe na Yeremia, wala mtu asipajue mlipo.