Yer. 32:23-40 Swahili Union Version (SUV)

23. nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lo lote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote;

24. angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona.

25. Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?

26. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema,

27. Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?

28. Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitautia mji huu katika mikono ya Wakaldayo, na katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atautwaa;

29. na Wakaldayo, wanaopigana na mji huu, watakuja, na kuutia moto mji huu, na kuuteketeza, pamoja na nyumba zake, ambazo juu ya dari zake wamemfukizia Baali uvumba, na kuwamiminia miungu mingine vinywaji, ili kunikasirisha.

30. Maana wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wametenda yaliyo mabaya tu mbele za uso wangu, tangu ujana wao; maana wana wa Israeli wamenichokoza tu kwa matendo ya mikono yao, asema BWANA.

31. Kwa kuwa mji huu umekuwa sababu ya kunitia hasira, na sababu ya ghadhabu yangu, tangu siku ile walipoujenga hata siku hii ya leo; ili niuondoe usiwe mbele za uso wangu;

32. kwa sababu ya mabaya yote ya wana wa Israeli, na ya wana wa Yuda, waliyoyatenda ili kunitia hasira, wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao, na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu.

33. Tena wamenigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao; ingawa naliwafundisha, niliondoka mapema na kuwafundisha, lakini hawakusikiliza ili wapate mafundisho.

34. Bali waliweka machukizo yao ndani ya nyumba iliyoitwa kwa jina langu, ili kuinajisi.

35. Tena walijenga mahali palipoinuka kwa Baali, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ili kuwapitisha wana wao na binti zao katika moto kwa ajili ya Moleki, jambo nisilowaagiza; wala halikuingia moyoni mwangu kwamba walitende chukizo hilo; wapate kumkosesha Yuda.

36. Basi sasa, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za mji huu, ambao ninyi mnasema juu yake maneno haya, Umetiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni;

37. Tazama, nitawakusanya, na kuwatoa katika nchi zote nilikowafukuza, katika hasira yangu, na uchungu wangu, na ghadhabu yangu nyingi; nami nitawaleta tena hata mahali hapa, nami nitawakalisha salama salimini;

38. nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao;

39. nami nitawapa moyo mmoja na njia moja, wapate kunicha sikuzote; kwa mema yao, na ya watoto wao baada yao;

40. nami nitafanya agano la milele pamoja nao, kwamba sitageuka wala kuwaacha, ili niwatendee mema; nami nitatia kicho changu mioyoni mwao, ili wasiniache.

Yer. 32