Yer. 32:21-33 Swahili Union Version (SUV)

21. ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu;

22. ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali;

23. nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lo lote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote;

24. angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona.

25. Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?

26. Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema,

27. Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?

28. Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitautia mji huu katika mikono ya Wakaldayo, na katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atautwaa;

29. na Wakaldayo, wanaopigana na mji huu, watakuja, na kuutia moto mji huu, na kuuteketeza, pamoja na nyumba zake, ambazo juu ya dari zake wamemfukizia Baali uvumba, na kuwamiminia miungu mingine vinywaji, ili kunikasirisha.

30. Maana wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wametenda yaliyo mabaya tu mbele za uso wangu, tangu ujana wao; maana wana wa Israeli wamenichokoza tu kwa matendo ya mikono yao, asema BWANA.

31. Kwa kuwa mji huu umekuwa sababu ya kunitia hasira, na sababu ya ghadhabu yangu, tangu siku ile walipoujenga hata siku hii ya leo; ili niuondoe usiwe mbele za uso wangu;

32. kwa sababu ya mabaya yote ya wana wa Israeli, na ya wana wa Yuda, waliyoyatenda ili kunitia hasira, wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao, na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu.

33. Tena wamenigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao; ingawa naliwafundisha, niliondoka mapema na kuwafundisha, lakini hawakusikiliza ili wapate mafundisho.

Yer. 32