10. Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani.
11. Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi;
12. na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika uwanda wa walinzi.
13. Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema,
14. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa muhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi.
15. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.
16. Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nalimwomba BWANA, nikisema,
17. Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza;
18. wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, BWANA wa majeshi ndilo jina lake;
19. mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake,
20. wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo;
21. ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu;
22. ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali;