Yer. 30:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,

2. BWANA Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia.

3. Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema BWANA; nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki.

4. Na haya ndiyo maneno aliyosema BWANA, katika habari za Israeli, na katika habari za Yuda.

5. Maana BWANA asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani.

6. Ulizeni sasa, mkaone kwamba mwanamume aona utungu wa uzazi; mbona, basi, ninaona kila mtu anaweka mikono yake viunoni, kama mwanamke aliye na utungu, na nyuso zote zimegeuka rangi.

7. Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo.

8. Na itakuwa katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena;

9. bali watamtumikia BWANA, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.

10. Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema BWANA; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.

11. Maana mimi ni pamoja nawe, asema BWANA, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu.

12. Maana BWANA asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa.

Yer. 30