Yer. 3:7-18 Swahili Union Version (SUV)

7. Nami nalisema baada ya yeye kuyatenda hayo yote, Atanirudia mimi, lakini hakurudi; na dada yake, Yuda mwenye hiana, akayaona hayo.

8. Nami nikaona, wakati nilipokuwa nimemwacha Israeli mwenye kuasi, nikampa hati ya talaka kwa sababu hiyo ya kuzini, dada yake, Yuda mwenye hiana, hakufanya hofu; bali yeye naye akaenda akafanya mambo ya ukahaba.

9. Hata ikawa, kwa sababu alikuwa mwepesi wa kufanya ukahaba, nchi ikatiwa unajisi, naye akazini na mawe na miti.

10. Na pamoja na hayo yote dada yake, Yuda mwenye hiana, hajanirudia mimi kwa moyo wake wote, bali kwa unafiki, asema BWANA.

11. BWANA, akaniambia, Israeli mwenye kuasi amejionyesha kuwa mwenye haki kuliko Yuda mwenye hiana.

12. Enenda, ukatangaze maneno haya kuelekea upande wa kaskazini, ukaseme, Rudi, Ee Israeli mwenye kuasi, asema BWANA; sitakutazama kwa hasira; maana mimi ni mwenye rehema, asema BWANA, sitashika hasira hata milele.

13. Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi BWANA, Mungu wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema BWANA.

14. Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema BWANA; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni;

15. nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.

16. Kisha itakuwa, mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo, asema BWANA, siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la BWANA; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena.

17. Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha BWANA; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la BWANA; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya.

18. Siku zile nyumba ya Yuda watakwenda pamoja na nyumba ya Israeli, nao watakuja pamoja, kutoka nchi ya kaskazini, mpaka nchi ile niliyowapa baba zenu iwe urithi wao.

Yer. 3