11. BWANA, akaniambia, Israeli mwenye kuasi amejionyesha kuwa mwenye haki kuliko Yuda mwenye hiana.
12. Enenda, ukatangaze maneno haya kuelekea upande wa kaskazini, ukaseme, Rudi, Ee Israeli mwenye kuasi, asema BWANA; sitakutazama kwa hasira; maana mimi ni mwenye rehema, asema BWANA, sitashika hasira hata milele.
13. Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi BWANA, Mungu wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema BWANA.
14. Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema BWANA; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni;
15. nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.
16. Kisha itakuwa, mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo, asema BWANA, siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la BWANA; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena.
17. Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha BWANA; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la BWANA; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya.
18. Siku zile nyumba ya Yuda watakwenda pamoja na nyumba ya Israeli, nao watakuja pamoja, kutoka nchi ya kaskazini, mpaka nchi ile niliyowapa baba zenu iwe urithi wao.
19. Lakini mimi nalisema, Nitawezaje kukuweka pamoja na watoto, na kukupa nchi ipendezayo, urithi ulio mwema wa mataifa? Nami nikasema, Mtaniita, Baba yangu, wala hamtageuka na kuacha kunifuata.
20. Hakika kama vile mke amwachavyo mumewe kwa hiana, ndivyo mlivyonitenda mimi kwa hiana, Ee nyumba ya Israeli, asema BWANA.
21. Sauti inasikiwa juu ya vilele vya milima, ni kulia kwao na maombi yao wana wa Israeli; kwa kuwa wameipotosha njia yao, wamemsahau BWANA, Mungu wao.
22. Rudini, enyi watoto waasi, mimi nitaponya maasi yenu. Tazama, tumekuja kwako; maana wewe u BWANA, Mungu wetu.
23. Ni kweli, msaada haufai unaotazamiwa kutoka milimani, makutano yenye mshindo juu ya milima; ni kweli, wokovu wa Israeli ni katika BWANA, Mungu wetu.