Yer. 3:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Watu husema, Mtu akimwacha mkewe, naye akienda zake, akawa mke wa mtu mwingine, je! Mtu huyo atamrudia tena? Je! Nchi hiyo haitatiwa unajisi? Lakini wewe umefanya mambo ya ukahaba na wapenzi wengi; nawe, je! Utanirudia mimi? Asema BWANA.

2. Inua macho yako, ukavitazame vilele vya milima, ukaone; pa wapi mahali ambapo hawakulala nawe? Kando ya njia umeketi ili kuwangojea, kama vile Mwarabu jangwani; nawe umeitia nchi unajisi kwa ukahaba wako na uovu wako.

3. Kwa sababu hiyo manyunyu yamezuiliwa, wala hapakuwa na mvua ya vuli; hata hivyo ulikuwa na kipaji cha uso cha kahaba, ulikataa kutahayarika.

4. Je, tokea wakati huu hutanililia, Ee Baba yangu, wewe u kiongozi wa ujana wangu?

5. Je! Ataishika hasira yake hata milele? Ataishika hata mwisho? Tazama, umesema hivyo, bali umetenda mambo mabaya, umefuata njia yako mwenyewe.

6. Tena, BWANA akaniambia siku za mfalme Yosia, Je! Umeyaona aliyotenda Israeli mwenye kuasi? Amepanda juu ya kila mlima mrefu, akafanya huko mambo ya ukahaba, tena, chini ya kila mti wenye majani mabichi.

7. Nami nalisema baada ya yeye kuyatenda hayo yote, Atanirudia mimi, lakini hakurudi; na dada yake, Yuda mwenye hiana, akayaona hayo.

8. Nami nikaona, wakati nilipokuwa nimemwacha Israeli mwenye kuasi, nikampa hati ya talaka kwa sababu hiyo ya kuzini, dada yake, Yuda mwenye hiana, hakufanya hofu; bali yeye naye akaenda akafanya mambo ya ukahaba.

9. Hata ikawa, kwa sababu alikuwa mwepesi wa kufanya ukahaba, nchi ikatiwa unajisi, naye akazini na mawe na miti.

Yer. 3