13. Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote.
14. Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.
15. Maana BWANA, Mungu wa Israeli, aniambia hivi, Pokea kikombe cha divai ya ghadhabu hii mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote, ambao nitakupeleka kwao;
16. nao watakunywa, na kulewalewa, na kufanya wazimu, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yao.
17. Ndipo nikakipokea kikombe kile mkononi mwa BWANA, nikawanywesha mataifa yote, ambao BWANA alinipeleka kwao;
18. yaani, Yerusalemu, na miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, ili kuwafanya kuwa ukiwa, na ajabu, na mazomeo, na laana; vile vile kama ilivyo leo;
19. Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote;
20. na watu wote waliochanganyika pamoja, na wafalme wote wa nchi ya Uzi, na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;
21. Edomu, na Moabu, na wana wa Amoni;
22. na wafalme wote wa Tiro, na wafalme wote wa Sidoni, na wafalme wote wa kisiwa kilicho ng’ambo ya pili ya bahari;
23. Dedani, na Tema, na Buzi, na watu wote wakatao denge;
24. na wafalme wote wa Arabuni, na wafalme wote wa watu waliochanganyika wakaao jangwani;
25. na wafalme wote wa Zimri, na wafalme wote wa Elamu, na wafalme wote wa Wamedi;
26. na wafalme wote wa kaskazini, walio mbali na walio karibu, wote pamoja; na wafalme wote wa dunia, wakaao juu ya uso wa dunia; na mfalme wa Sheshaki atakunywa baada yao.
27. Nawe utawaambia hivi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyweni, na kulewa, na kutapika, na kuanguka msiinuke tena, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yenu.
28. Tena itakuwa, kama wakikataa kukipokea kikombe kile mkononi mwako, wanywe, ndipo utakapowaambia, BWANA wa majeshi asema hivi, Lazima mtakunywa.
29. Maana angalieni, ninaanza kutenda mabaya katika mji uitwao kwa jina langu, je! Mtaachiliwa ninyi msiadhibiwe? Hamtaachiliwa msiadhibiwe; kwa maana nitauita upanga ule uwapige wote wakaao katika dunia, asema BWANA wa majeshi.