10. Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa.
11. Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.
12. Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema BWANA, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele.
13. Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote.
14. Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.
15. Maana BWANA, Mungu wa Israeli, aniambia hivi, Pokea kikombe cha divai ya ghadhabu hii mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote, ambao nitakupeleka kwao;
16. nao watakunywa, na kulewalewa, na kufanya wazimu, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yao.
17. Ndipo nikakipokea kikombe kile mkononi mwa BWANA, nikawanywesha mataifa yote, ambao BWANA alinipeleka kwao;
18. yaani, Yerusalemu, na miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, ili kuwafanya kuwa ukiwa, na ajabu, na mazomeo, na laana; vile vile kama ilivyo leo;
19. Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote;
20. na watu wote waliochanganyika pamoja, na wafalme wote wa nchi ya Uzi, na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;
21. Edomu, na Moabu, na wana wa Amoni;
22. na wafalme wote wa Tiro, na wafalme wote wa Sidoni, na wafalme wote wa kisiwa kilicho ng’ambo ya pili ya bahari;