1. Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, katika habari za watu wote wa Yuda; katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda mwaka ule ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli;
2. ambalo Yeremia, nabii, aliwaambia watu wote wa Yuda, na wenyeji wote wa Yerusalemu, kusema,
3. Tangu mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, hata siku hii ya leo, miaka hii ishirini na mitatu, neno la BWANA limenijia, nami nimesema nanyi, nikiamka mapema na kusema; lakini ninyi hamkusikiliza.
4. Naye BWANA ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize.
5. Akasema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya; uacheni uovu wa matendo yenu, mkae katika nchi ambayo BWANA aliwapa, ninyi na baba zenu, tangu zamani za kale na hata milele;
6. wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia na kuwasujudia, wala msinikasirishe kwa kazi ya mikono yenu; basi, mimi sitawadhuru ninyi kwa dhara lo lote.