Yer. 23:29-40 Swahili Union Version (SUV)

29. Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?

30. Basi kwa sababu hiyo mimi ni juu ya manabii hao, asema BWANA, wanaompokonya kila mtu jirani yake maneno yangu.

31. Tazama, mimi ni juu ya manabii, asema BWANA, wanaotumia ndimi zao na kusema, Yeye asema,

32. Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA.

33. Na watu hawa, au nabii au kuhani, atakapokuuliza, akisema, Mzigo wa BWANA ni nini? Ndipo utawaambia, Mzigo gani? BWANA asema, Nitawatupilia mbali.

34. Na katika habari ya nabii, na kuhani, na watu, watakaosema, Mzigo wa BWANA, mimi nitamwadhibu mtu yule, na nyumba yake.

35. Mtasema hivi kila mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu yake, BWANA amejibu mtu? Na, BWANA amesemaje?

36. Na mzigo wa BWANA hamtautaja tena; maana neno la kila mtu ndilo litakalokuwa mzigo wake; maana ninyi mmeyapotosha maneno ya Mungu aliye hai, ya BWANA wa majeshi, Mungu wetu.

37. Nawe utamwambia nabii hivi, BWANA amekujibu nini? Na, BWANA amesemaje?

38. Lakini mkisema, Mzigo wa BWANA, basi, BWANA asema hivi, Kwa sababu mwasema neno hili, “Mzigo wa BWANA”; nami nimemtuma mtu kwenu kusema, Msiseme, “Mzigo wa BWANA”;

39. basi, kwa hiyo angalieni, nitawasahau ninyi kabisa, nami nitawatupilia mbali, pamoja na mji huu niliowapa ninyi na baba zenu, mtoke mbele za uso wangu;

40. nami nitaleta juu yenu aibu ya milele, na fedheha ya daima, ambayo haitasahauliwa.

Yer. 23