Yer. 23:1-15 Swahili Union Version (SUV)

1. Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema BWANA.

2. Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema BWANA.

3. Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka.

4. Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema BWANA.

5. Tazama siku zinakuja, asema BWANA, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi.

6. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA ni haki yetu.

7. Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema BWANA, ambapo hawatasema tena, Aishivyo BWANA, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri;

8. lakini, Aishivyo BWANA, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.

9. Katika habari za manabii.Moyo wangu ndani yangu umevunjika,Mifupa yangu yote inatikisika.Nimekuwa kama mtu aliye mlevi,Na kama mtu aliyeshindwa na divai;kwa ajili ya BWANA, na kwa ajili ya maneno yake matakatifu.

10. Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.

11. Maana nabii, na kuhani, wote wawili wanakufuru; naam, katika nyumba yangu nimeuona uovu wao, asema BWANA.

12. Kwa ajili ya hayo njia yao itakuwa kwao kama mahali pa kuteleza gizani; watatelemshwa na kuanguka hapo; kwa maana nitaleta uovu juu yao, naam, mwaka wa kujiliwa kwao, asema BWANA.

13. Nami nimeona upumbavu katika manabii wa Samaria; walitabiri kwa Baali, wakawakosesha watu wangu Israeli.

14. Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.

15. Basi BWANA wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.

Yer. 23