17. Usiwe sababu ya hofu kuu kwangu mimi; wewe ndiwe uliye kimbilio langu siku ya uovu.
18. Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.
19. BWANA akaniambia hivi, Enenda ukasimame katika lango la wana wa watu hawa, waingiapo wafalme wa Yuda, na watokeapo, na katika malango yote ya Yerusalemu,
20. ukawaambie, Lisikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda, na Yuda wote, nanyi wenyeji wote wa Yerusalemu, ninyi mwingiao kwa malango haya;
21. BWANA asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue mzigo wo wote siku ya sabato, wala msiulete ndani kwa malango ya Yerusalemu;
22. wala msitoe mzigo katika nyumba zenu siku ya sabato, wala msifanye kazi yo yote; bali itakaseni siku ya sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu;
23. lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, ili wasisikilize wala wasipokee mafundisho.