3. Maana BWANA asema hivi, katika habari za wana, na katika habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na katika habari za mama zao waliowazaa, na katika habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii;
4. watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.
5. Maana BWANA asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema BWANA, hata fadhili zangu na rehema zangu.
6. Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikata-kata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao;
7. wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao.
8. Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa.
9. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi, mbele ya macho yenu, na katika siku zenu, nitaikomesha sauti ya furaha, na sauti ya kicheko, mahali hapa; sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi.
10. Tena itakuwa, utakapowaonyesha watu hawa maneno haya yote, nao wakakuambia, Mbona BWANA amenena juu yetu mabaya haya makuu? Uovu wetu ni uovu gani? Na dhambi yetu, tuliyomtenda BWANA, Mungu wetu, ni nini?
11. Ndipo utakapowaambia, Ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema BWANA, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu;
12. na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaenenda kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi;
13. basi, kwa sababu hiyo, nitawatoeni katika nchi hii, na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu; na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku; kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo.