10. Tena itakuwa, utakapowaonyesha watu hawa maneno haya yote, nao wakakuambia, Mbona BWANA amenena juu yetu mabaya haya makuu? Uovu wetu ni uovu gani? Na dhambi yetu, tuliyomtenda BWANA, Mungu wetu, ni nini?
11. Ndipo utakapowaambia, Ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema BWANA, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu;
12. na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaenenda kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi;
13. basi, kwa sababu hiyo, nitawatoeni katika nchi hii, na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu; na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku; kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo.
14. Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema BWANA, ambapo hawatasema tena, Aishivyo BWANA, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;
15. lakini, Aishivyo BWANA, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza; nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe niliyowapa baba zao.
16. Tazama, asema BWANA, Nitatuma watu kuwaita wavuvi wengi, nao watawavua; na baada ya hayo nitatuma watu kuwaita wawindaji wengi, nao watawawinda, watoke katika kila mlima, na kila kilima, na pango za majabali.
17. Maana macho yangu yaziangalia njia zao zote, hawakufichwa uso wangu usiwaone, wala haukusitirika uovu wao macho yangu yasiuone.
18. Nami kwanza nitawalipa uovu wao na dhambi zao maradufu, kwa kuwa wameitia unajisi nchi yangu, kwa mizoga ya vitu vyao vichukizavyo, na kuujaza urithi wangu kwa machukizo yao.
19. Ee BWANA, nguvu zangu, ngome yangu, na kimbilio langu siku ya taabu, kwako wewe watakuja mataifa yote toka ncha za dunia, wakisema, Baba zenu hawakurithi kitu ila uongo, naam, ubatili na vitu visivyofaa.