6. Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi;
7. katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu,
8. na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.
9. Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wenye kujibu,
10. wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.
11. Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;
12. nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;
13. tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;
14. ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.
15. Nena maneno hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote.