1. Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima;
2. ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi.
3. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;
4. ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;
5. na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.