Tit. 1:7-15 Swahili Union Version (SUV)

7. Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu;

8. bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake;

9. akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.

10. Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao.

11. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.

12. Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, hayawani wabaya, walafi wavivu.

13. Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani;

14. wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu wajiepushao na yaliyo kweli.

15. Vitu vyote ni safi kwa hao walio safi; lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini; bali akili zao zimekuwa najisi, na nia zao pia.

Tit. 1