1. Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi.
2. Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi.
3. Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki;
4. nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi.