Rum. 9:16-24 Swahili Union Version (SUV)

16. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.

17. Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.

18. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.

19. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?

20. La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?

21. Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?

22. Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;

23. tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;

24. ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia?

Rum. 9