2. Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume.
3. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.
4. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.
5. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.
6. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.
7. Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.
8. Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa.