Rum. 3:11-28 Swahili Union Version (SUV)

11. Hakuna afahamuye;Hakuna amtafutaye Mungu.

12. Wote wamepotoka, wameoza wote pia;Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.

13. Koo lao ni kaburi wazi,Kwa ndimi zao wametumia hila.Sumu ya fira i chini ya midomo yao.

14. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.

15. Miguu yao ina mbio kumwaga damu.

16. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao.

17. Wala njia ya amani hawakuijua.

18. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.

19. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu;

20. kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.

21. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii;

22. ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;

23. kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;

24. wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;

25. ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa;

26. apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.

27. Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.

28. Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.

Rum. 3