17. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu.
18. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo,
19. kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu;
20. kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine;
21. bali kama ilivyoandikwa,Wale wasiohubiriwa habari zake wataona,Na wale wasiojasikia watafahamu.
22. Ndiyo sababu nalizuiwa mara nyingi nisije kwenu.
23. Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena tangu miaka mingi nina shauku kuja kwenu;
24. wakati wo wote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana nataraji kuwaona ninyi katika kusafiri kwangu, na kusafirishwa nanyi, moyo wangu ushibe kwenu kidogo.
25. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu;
26. maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini.
27. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili.
28. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia muhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania.
29. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo.