1. Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata;Utazame na kuiona aibu yetu.
2. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni;Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.
3. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba;Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4. Tumekunywa maji yetu kwa fedha;Kuni zetu twauziwa.
5. Watufuatiao wa juu ya shingo zetu;Tumechoka tusipate raha yo yote.
6. Tumewapa hao Wamisri mkono;Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7. Baba zetu walitenda dhambi hata hawako;Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8. Watumwa wanatutawala;Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9. Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu;Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10. Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu;Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.
11. Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni;Na mabikira katika miji ya Yuda.
12. Wakuu hutungikwa kwa mikono yao;Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13. Vijana huyachukua mawe ya kusagia;Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14. Wazee wameacha kwenda langoni;Na vijana kwenda ngomani.
15. Furaha ya mioyo yetu imekoma;Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16. Taji ya kichwa chetu imeanguka;Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17. Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia;Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18. Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa,Mbweha hutembea juu yake.
19. Wewe, BWANA, unadumu milele;Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20. Mbona watusahau sikuzote;Na kutuacha muda huu mwingi?
21. Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22. Isipokuwa wewe umetukataa kabisa;Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.