8. nawe ukauona moyo wake kuwa mwaminifu mbele zako, ukafanya agano naye, kumpa nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Myebusi, na Mgirgashi, naam, kuwapa wazao wake; nawe umeyafikiliza maneno yako, kwa kuwa ndiwe mwenye haki.
9. Tena uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya bahari ya Shamu;
10. nawe ukaonyesha ishara nyingi na mambo ya ajabu juu ya Farao, na juu ya watumishi wake wote, na juu ya watu wote wa nchi yake; kwa maana ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina kama vile ilivyo leo.
11. Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, mfano wa jiwe katika maji makuu.
12. Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.
13. Tena ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;
14. ukawajulisha sabato yako takatifu, na kuwaagiza maagizo, na amri, na sheria, kwa mkono wa mtumishi wako, Musa.
15. Ukawapa chakula toka mbinguni, kwa ajili ya njaa yao, na kwa ajili yao ukaleta maji kutoka mwambani, kwa sababu ya kiu yao, ukawaamuru kwamba waingie katika nchi na kuimiliki, ambayo umeinua mkono wako kuwapa.