1. Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao, juu ya ndugu zao Wayahudi.
2. Maana, walikuwako watu waliosema, Sisi, na wana wetu na binti zetu, tu wengi; na tupate ngano, tule, tukaishi.
3. Tena walikuwako wengine waliosema, Tumeweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu, na nyumba zetu; tupate ngano, kwa sababu ya njaa.
4. Tena walikuwako wengine waliosema, Tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu.
5. Walakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe! Mnawatia utumwani wana wetu na binti zetu kuwa watumishi, na baadhi ya binti zetu wamekwisha kutiwa utumwani; wala hatuwezi kujiepusha na hayo; maana watu wengine wana mashamba yetu na mizabibu yetu.
6. Nami nilikasirika sana, niliposikia kilio chao, na maneno hayo.