6. Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.
7. Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno;
8. wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.
9. Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu, tena tukaweka walinzi, mchana na usiku, kwa sababu yao, ili kuwapinga.
10. Wakasema Yuda, Nguvu zao wachukuao mizigo zimedhoofika, na kifusi tele zipo; tusiweze kuujenga ukuta.
11. Nao adui zetu wakasema, Hawatajua wala kuona, hata tutakapokuja kati yao, na kuwaua, na kuikomesha kazi hiyo.
12. Kisha ikawa, Wayahudi walipokuja, wale waliokaa karibu nao, wakatuambia mara kumi, Kutoka kila mahali mtakaporejea watatushambulia.
13. Basi, nikaweka watu, mahali pa chini pa nafasi iliyokuwa nyuma ya ukuta, mahali palipokuwa wazi, kwa kadiri ya jamaa zao, nikawaweka wenye panga zao, na mikuki yao, na pinde zao.
14. Nikatazama, nikaondoka, nikawaambia wakuu, na mashehe, na watu wengine waliobaki, Msiwaogope; mkumbukeni Bwana, aliye mkuu mwenye kuogofya, mkawapiganie ndugu zenu, na wana wenu, na binti zenu, na wake zenu, na nyumba zenu.
15. Kisha ikawa, adui zetu waliposikia ya kuwa tumekwisha kupata habari, na ya kuwa Mungu amelibatilisha shauri lao, ndipo sisi sote tukarudi ukutani, kila mtu kwa kazi yake.
16. Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.
17. Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;
18. nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.
19. Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;