6. Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi.
7. Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika.
8. Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi,
9. wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, mume na mke, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu.
10. Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi.
11. Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka.
12. Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku.
13. Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye;
14. wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote.
15. Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake.
16. Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia.
17. Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi.
18. Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji.