Mwa. 50:1-7 Swahili Union Version (SUV)

1. Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu.

2. Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga, kwamba wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli.

3. Siku zake arobaini zikaisha, maana hivyo hutimizwa siku za kupaka dawa. Wamisri wakamlilia siku sabini.

4. Siku za kumlilia zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema,

5. Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi.

6. Farao akasema, Uende, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha.

7. Basi Yusufu akaenda amzike babaye, na watumwa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri.

Mwa. 50